Pages

Tuesday, August 7, 2012

INTERVIEW YA NANCY SUMARY: OLD IS GOLD....... HAPPY BIRTHDAY MDADA


Ikiwa leo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mrembo Nancy Sumary, tujikumbushe mahojiano aliyowahi kuyafanya mwaka 2005 ambapo alifanya vizuri sana kwenye maswala ya urembo. Twende pamoja hapo chini kufuatilia mahojiano hayo
 Lengo likiwa ni kuonyesha kuwa Nancy Sumary alijiamini kwa kiasi gani na mwenye matumaini makubwa wakati wa maandalizi yake kuelekea Miss World, na alipewa sapoti ya kiasi gani na kamati ya Miss Tanzania ili angalau aweze kufanya vizuri katika shindano hilo.

Baada ya mawasiliano ya hapa na pale na mkurugenzi wa kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga ndipo nilipokutana na MissTanzania Nancy Sumari kwenye ofisi za kamati hiyo zilizopo jengo la Mavuno House, ghorofa ya nne na kufanya mahojiano naye kama ifuatavyo.
Mwandishi : Miss Tanzania Nancy Sumary hujambo dada?.

Nancy : Mimi sijambo kaka namshukuru Mungu.

Mwandishi : Tunaomba utupe historia yako kwa ufupi.

Nancy : Anatoa kicheko na kuonyesha tabasamu la kuvutia huku akianza kwa kusema “Mimi nimezaliwa miaka 19 iliyopita na nimepata elimu yangu nchini kenya, ambapo nilisoma huko mpaka kidato cha nne katika shule inayoitwa Maasai High School.”
Mwandishi : Kama unavyojua unakabiliwa na kazi ngumu ya kuwatoa kimasomaso Watanzania kwenye shindano la Miss World vipi maandalizi yako yamefikia wapi hivi sasa.?

Nancy : Kwa ujumla maandalizi sio mabaya yanaendelea vizuri na ninapata msaada mkubwa kutoka kamati ya Miss Tanzania nafikiri nitafanya vizuri tu.

Mwandishi : Unaweza kutupa ratiba yako ya kila siku jinsi unavyoipanga na kuifanyia kazi katika kujiandaa.?
Nancy : Ili kufanikisha jambo lolote unalotaka kulifanya hasa kitu kama mashindano unahitaji kuwa na utaratibu mzuri wa kujiandaa ili uweze kufanya vizuri, na mimi pia nimepewa ratiba ambayo ninaitumia katika kujiandaa kwangu.
“Nikiamka asubuhi ili kujiweka fiti huwa nafanya mazoezi ya kuruka kamba mara 200 au 300 hivi, zoezi ambalo hunichangamsha na kuniweka sawa kwa lolote ambalo ninatarajia kulifanya katika ratiba yangu inayofuata.
Jambo la pili huwa ninaoga baada ya kuoga ninakunywa chai kikombe kimoja na mkate na yai moja, baada ya hapo ninakunywa juisi glasi moja, lakini pia huwa nabadilisha chakula kutokana na ratiba inavyosema siku hiyo.
Jambo la tatu huwa nawasiliana na ofisi ya kamati ya Miss Tanzania ili kujua ratiba ya shuguli za ofisi hiyo ambazo natakiwa kuzifanya kwa siku hiyo, ikiwa pia kukutana na mshauri wa kamati ya Miss Tanzania katika masuala ya urembo Dk. Ramesh ambaye hunishauri mambo mbalimbali yanayofanyika kwenye shindano la Miss World na kuniandaa kisaikolojia.
Jambo la nne ninalolifanya baada ya hapo ni kupata chakula cha mchana, nikishakula huwa napata muda kidogo wa kupumzika halafu baadae naingia kwenye Internet cafe', natafuta mtandao wa Miss World na kusoma habari mbalimbali za shindano hilo ili kujua vitu kadhaa juu ya mashindano na kuwajua warembo kutoka mataifa mbalimbali nitakaoshindana nao siku hiyo ya Miss World.
Inapofika jioni ninakwenda Gym kwa ajiri ya kufanya mazoezi mbalimbali ya kurekebisha na kuweka sawa mwili wangu tayari kwa hayo mashindano ya Miss World.

Mwandishi : Vipi kuhusu suala zima la mavazi kwa ajili ya shindano, umefikia wapi.?

Nancy : Nguo zangu zote nitakazozitumia kwenye Miss World nitazinunua huko Dubai ambako ndiko nitafanyia Shoping yangu kwa ajili ya mashindano.

Mwandishi : Kila mtu huwa ana vitu ambavyo huwa anavipendelea maishani mwake katika burudani, je wewe unapenda nini.?

Nancy : Mimi napenda kuangalia sinema, kusikiliza muziki kama vile Hip Hop na R&B, mpira wa miguu, lakini pia napenda kudansi kama vile kwenda club ambako huwa naenda na dada yangu anayeitwa Grolia.

Mwandishi : Je, kuna jambo lingine lolote la ziada ambalo unalifanya kwa ajili ya maandalizi yako.?

Nancy : Ndiyo unajua mimi sitishiki na wala sikatishwi tamaa na matokeo ya warembo wenzangu waliowahi kunitangulia katika mashindano hayo, kwani nimejiandaa vya kutosha kuionyesha Dunia kwamba Watanzania ni watu wenye kujiamini wenye ustaarabu na ukarimu, kwa hiyo ninaamini kuwa Mungu atanisaidia, nitafanya maajabu huko Sanya, lakini pia nashukuru kwamba kamati ya Miss Tanzania imenisapoti kwa kiasi kikubwa katika maandalizi yangu kwa ujumla.
Mwandishi ; Nini mipango yako mara utakaporejea kutoka katika mashindano ya Miss World.?
Nancy : Kama nilivyosema hapo mwanzonkua ninaamini nitafanya vizuri katika shindani hilo, hivyo nadhani nitakua na kazi kubwa ya kufanya hasa kuwapa moyo warembo wenzangukuwa Watanzania tukijiamini katika kila jambo tunao uwezo wa kufanya vizuri.
Lakini pia nitakaporejea pamoja na kazi zingine za kijamii ninataka kufanya kazi zaidi na vijana wenzangu ambapo natarajia kutoa mawazo, elimu na kuwahamasisha vijana juu ya kupenda elimu kupitia makongamano, kwani elimu ndiyo ukombozi wa kweli kwa vijana. Pia natarajia kuendelea na elimu ya juu na nitaanzia na Diploma ya sheria na hapo baadae Digrii.
Nancy Sumari ni mrembo aliyenishangaza kiasi fulani wakati nilipokuwa nazungumza naye, kwani alizungumza kwa ujasiri na kujiamini kwa kiasi kikubwa kana kwamba alikua haoni uzito na ushindani wa warembo wenzie katika shinano la Miss World. Sijui alipata wapi ujasiri huo, ukizingatia kwamba tangu mwaka 1994 tulipoanza kushiriki, warembo wetu wamekuwa wakiingia kwenye shindano hilo kama wasindikizaji tu kutokana na kufanya vibaya kila mwaka.
Ni kama vile Nancy Abraham Sumary alibashiri kitakachotokea huko Sanya, na kweli ndivyo ilivyotokea kwani amefanikiwa kuingia kwenye sita bora ya Miss World na kuchukua taji la Miss World Africa baada ya kumshinda mrembo mwenzie kutoka Africa ya kusini, Dhiveja Sundrum hivyo kuitangaza na kuipatia sifa kubwa Tanzania katika masuala ya urembo Duniani.
Pamoja na Nancy mwenyewe kujiamini kiasi hicho lakini wadau wengi wa urembo nchini ikiwemo kamati ya Miss Tanzania yenyewe na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini vilionekana kukata tamaa. Hiyo ilitokana na mambo yalivyokua yakienda hasa baada ya Miss World kutangaza kubadili taratibu za namnaya kuwapata washindi kwa kutumia Credit Card, kitu ambacho hata Mkurugenziwa kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga alitamka wazi mbale ya waandishi wa habari kuwa hakuna matumaini kwa Nancy kufanya vizuri huko Sanya.
Hata hivyo sasa ni wakati wa kufurahia mafanikio haya ya Nancy na kuyazika mawazo yote, kwamba warembo wa Tanzania ni wasindikizaji tu katika mashindano ya Miss World. Nancy ameionyesha Dunia kua Watanzania wanaweza kama alivyoeleza hapo awali wakati alpokuwa akijiandaa kwenda huko Sanya China,Hongera sana Nancy Abraham Sumary Miss World Africa kwa kuibeba Tanzania katika sanaa ya urembo 

SOURCE: KITANGOMA MAGAZINE VOL 1 TOLEO NAMBA  012

HAPPY BIRTHDAY NANCY SUMARY......MUNGU AKUPE UHAI MREFU

1 comment: